KIJIJI cha Msitu wa Mbogo wilayani Arumeru mkoani Arusha, jana kililipuka kwa furaha baada ya viongozi wanne wa kijiji hicho, akiwemo mwenyekiti, kuachiwa huru kwa dhamana na Mahakama.
Waliachiwa baada ya siku 20 za vilio, simanzi na majonzi za wakazi wa kijiji hicho kuhusu suala la viongozi hao. Viongozi hao, Mwenyekiti wa Kijiji, Ernest Mkilanyi na wajumbe wake wanne, walihukumiwa jumla ya miaka 75 jela hivi karibuni kwa unyang’anyi wa Sh 780,000.
Kila mtu alihukumiwa miaka 15 jela. Kuachiwa kwa dhamana kwa viongozi hao kunatokana na juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Husna Mwilima na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama katika kushughulikia rufaa dhidi ya hukumu hiyo, iliyotolewa na Hakimu John Mwita wa Mahakama ya Mwanzoya Mbuguni/Maji ya Chai .
Mwilima aliwaahidi wananchi hao, walipoandamana hadi ofisini kwake Aprili 10 mwaka huu kupinga hukumu hiyo na kumuomba kuwapatia tena viongozi wao kwa kuwarejesha uraiani.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara na mapokezi ya mwenyekiti huyo na viongozi wenzake wa Serikali ya Kijiji, Mkuu huyo wa Wilaya alisema yeye na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama waliamua kuingilia kati hukumu hiyo kwa kukata rufaa,
kutokana na kutoridhishwa na mwenendo mzima wa kesi. Alisema anatambua Mahakama ni mhimili kati ya mihimili mitatu ya nchi unaojitegemea, lakini aliutaka kutenda haki katika kazi zake na wao kama mhimili mwingine ambao ni serikali, hautasita kuingilia kati jambo ambalo wataliona halijakwenda sawa.
Mkuu huyo aliongeza kuwa, kutokana na mazingira ya kesi hiyo aliwaagiza Mwanasheria wa Halmashauri, Katibu Tawala wa Wilaya na Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wilayani humo, kufuatilia jambo hilo na kuweka mazingira ya kukata rufaa.
Alisema kazi hiyo ilifanyika vyema na ndipo wawili kati ya watuhumiwa hao watano, Julius Nyangusi na Edwin Deo walipofutiwa hukumu na kuachiwa huru, kwa kuwa hawakuhudhuria mahakamani hata siku moja tangu kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa.
Mwilima alisema kutokana na rufaa hiyo kukubaliwa, ndipo walipowasilisha maombi mengine ya kuachiwa kwa dhamana washitakiwa wawili wakati rufaa yao ikisikilizwa, ambao ni mwenyekiti huyo na Juma Maulid, wakati Simon Simon akiendelea kubaki gerezani, kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya mauaji.
Hata hivyo kutokana na mazingira ya kesi yenyewe, wataendelea kuishughulikia kwa kuwa imegubikwa na mazingira yasiyoeleweka dhidi ya watuhumiwa na harakati walizokuwa wakizifanya dhidi ya mwekezaji wa shamba la Tanzania Plantation, Pradep Zodia na masuala ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwaeleza wananchi hao kuwa tayari timu kutoka Wizara ya Ardhi imeshawasili wilayani humo, kuanza kufanyia kazi mgogoro huo na aliwataka wawe watulivu wakati kazi hiyo ikiendelea.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya alifananisha tukio hilo la kuhukumiwa miaka 15 jela kuwa ni sawa na Yona katika kitabu cha Biblia, ambaye alimezwa na samaki na kisha kutemwa tena na kwamba kamwe hatarudi nyuma kutokana na vitisho hivyo.
Aidha, aliwataka wananchi wake kuwa watulivu katika kipindi cha kusikilizwa kwa rufaa yake kwa kuachana na matendo, ambayo yanaweza kuharibu mwenendo wa kesi hiyo na kuonekana yamefanyika kwa yeye kuwatuma au kwa sababu yupo nje kwa dhamana
Comments
Post a Comment