Magufuli ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kukabidhi maeneo ya barabara yaliyokamilika ya mradi wa barabara wa mabasi yaendayo kasi kwa Wakala wa Usafiri Haraka wa Mabasi(DART) ili yaanze kutumiwa na wananchi.
Aidha ameiagiza kampuni inayojenga mradi huo ya Strabag kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo haraka ambapo hadi sasa umekamilika kwa asilimia 90.
Dk Magufuli aliyasema hayo jana Dar es Salaam baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kutoka Morocco - Magomeni - Fire hadi Kariakoo na kuweka jiwe la msingi katika Barabara ya Uhuru.
Pia aliiagiza DART kuhakikisha mchakato wa kupata magari ili wanapokabidhiwa barabara hizo magari yaanze kufanya safari badala ya kupoteza muda mwingine wa kusubiri mabasi.
Alisema Dar es Salaam ni Mkoa ambao unatekeleza miradi mingi ya miundombinu ambapo kwa miradi inayotekelezwa kwa sasa na inayotarajiwa kujengwa inakaribia thamani ya Sh trilioni nne.
Alisema katika mradi wa barabara za juu zabuni zitafunguliwa mwaka huu na ambapo pia fedha za ujenzi wa daraja la Selander litakalopita baharini zimeshapatikana na ujenzi wake utaanza mwaka huu.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema mradi huo umepangwa kutekelezwa katika awamu sita, ambapo katika awamu ya kwanza umekamilika kwa asilimia 90 na utagharimu Sh bilioni 369 ambazo zinatolewa na Benki ya Dunia kama mkopo wa riba nafuu.
Disqus seems to be taking longer than usual. Reload?
Comments
Post a Comment