TABIA ya vijana wa sasa ya kuchukua fedha kutoka kwa wazee na kuwagawia vijana wenzao ili kurahisisha mambo kwa wazee hao, imeonesha kumkera Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na vijana mjini hapa alisema vijana wa zamani walikuwa tofauti na wa sasa, wakati vijana wakihakikisha mambo yanakwenda vyema na hawatumiki vibaya, wa sasa ndio wanachukua fedha na kuwagawia wenzao.
Alisema tabia ya baadhi ya viongozi wa vijana kutumika kugawa fedha za wazee inaua demokrasia na maadili na kuingiza utamaduni wa hovyo katika siasa.
“Kama ukiwa na viongozi wa vijana unapojihusisha na kugawa fedha, vijana hamuwezi kugeuka makuwadi, hamuwezi kugeuka kuwa mawakala wa kuhonga vijana wenzenu mtakuwa mmetoka kabisa kwenye mstari,” alisema Rais Kikwete.
Alikuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu jana huku akitamba kuwa CCM itaendelea kuongoza na wataisoma namba.
Aliwaasa vijana kuwa hatima ya CCM iko mikononi mwao na hivyo ni vyema wakajiepusha na matendo ya rushwa na ukiukaji wa maadili.
“Hatma ya CCM iko mikononi mwa vijana, Umoja wa Vijana una kazi ya kuandaa vijana, nina masikitiko kwa haya yanayotokea,” alisema.
Alisema shirikisho ni kiungo muhimu kati ya CCM na wanafunzi kwani wanachagua viongozi wa kutengeneza daraja kati ya wanafunzi na chama.
Alisema Umoja wa Vijana una kazi ya kuandaa vijana, kupata wanachama wapya na kuimarisha umoja huo ili uwe na manufaa hapo baadaye
Comments
Post a Comment