KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ameutaka uongozi wa timu yake kuhakikisha wanafanya usajili makini ili msimu ujao waweze kufanya vizuri na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Simba imemaliza nafasi ya tatu kwenye ligi ya msimu huu uliomalizika Jumamosi iliyopita na kufanya timu hiyo kumaliza nafasi nje ya mbili bora msimu wa tatu mfululizo na kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Akizungumza na gazeti hili jana Mkude alisema usajili makini ndiyo utakaobadili mwenendo mbaya wa timu hiyo na kurudisha furaha kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu yao ambao kwa muda mrefu imepotea.
“Simba ni timu kubwa, inaumiza kuona tunashindwa kumaliza japo nafasi ya pili naushauri uongozi kuwa makini katika usajili wa msimu ujao ili tubadili mwenendo wetu na kuwa bora kama ilivyokuwa siku za nyuma,” alisema Mkude.
Alisema sehemu kubwa ambayo angependa ifanyiwe marekebisho ni safu ya ulinzi na ushambuliaji ambazo zimeonesha upungufu mkubwa kwenye msimu uliomalizika kwa timu yao kushindwa kutimiza lengo walilojiwekea.
“Pamoja na kuanza vibaya, lakini baadaye tulibadilika na kuweka malengo ya kumaliza angalau nafasi ya pili, lakini pia haikutimia mapungufu yetu makubwa yalikuwa kwenye ulinzi na hata safu ya ushambuliaji ambayo imekosa mshambuliaji wa kuaminika,” alisema Mkude.
Safu ya ulinzi ya Simba msimu uliopita imeruhusu mabao 18 huku ile ya ushambuliaji ikufunga mabao 36 na mshambuliaji wake Emmanuel Okwi, akifunga mabao 10 wakati Ibrahim Ajibu akifunga mabao saba pekee.
Mkude alisema matumaini yake ni kuwa huu ndiyo msimu wa mwisho kupata matokeo mabaya na kumaliza nje ya mbili bora kwenye Ligi ya Bara kutokana na maandalizi pamoja na usajili wanaotarajia kuufanya
Comments
Post a Comment