MAKAMU wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amewataka wakazi wa Jiji la Arusha kuwa na mshikamano wa dhati katika kusimamia suala la amani kwani amani ikipotea hali ya uchumi itayumba.
Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa niaba ya Makamu wa Rais katika harambee ya ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha kiislamu iliyofanyika katika viwanja vya msikiti mkuu wa Ijumaa Jijini Arusha.
Alisema Jiji la Arusha ni la kitalii lenye muingiliano wa wageni wengi ambao lengo lao ni kwenda kutalii katika mbuga za wanyama hivyo wageni hao hawawezi kukubali kuja nchini hususan katika Jiji la Arusha kama kutakuwa na vurugu na watu kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.
Dk Bilal aliwataka wakazi wa Jiji la Arusha kuilinda amani kwa gharama yoyote na kushikamana bila ya kujali dini, kabila wala rangi kwani misingi iliyowekwa ni kwa kila mmoja kumheshimu mwenzake kwa kila namna.
Shehe wa Mkoa wa Arusha, Shabani Juma alisema kuwa lengo la harambee hiyo ni kutaka kukusanya zaidi ya Sh milioni 200 kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule ya sekondari itakayojengwa Patandi Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Shehe Juma alisema kuwa shule hiyo ambayo itakuwa chini ya Baraza Kuu la Kiislamu nchini (BAKWATA) itakuwa ya wanafunzi wa dini zote na itakuwa ndani ya kituo cha watoto yatima.
Makamu wa Rais na Lowassa na viongozi wengine wa serikali wamechangia harambee hiyo Sh milioni 105 na zaidi ya Sh milioni 140 zimekusanywa katika harambee hiyo zilizotolewa na wafanyabiashara na wanasiasa mbalimbali wa mkoani Arusha na nje ya mkoa.
Comments
Post a Comment