RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kuwa hana mpango wa kumfukuza Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mart Nooij.
Kwa sasa wadau mbalimbali wa soka wamependekeza kufukuzwa kwa kocha huyo hasa kutokana na kufanya vibaya kwa timu hiyo katika michuano ya Cosafa inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Timu hiyo inashiriki michuano hiyo kama mgeni mwalikwa ikiwa pamoja na Ghana, ilifungwa na Madagascar mabao 2-0 katika mchezo wake wa pili wa Kundi B uliofanyika kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng mjini Rustenburg.
Awali, Jumatatu wiki hii ilifungwa bao 1-0 na Swaziland katika mechi ya kwanza, hali ambayo inamaanisha kuwa timu hiyo haikupata hata bao moja, kitu ambacho kimewakera mashabiki wengi wa soka.
Lakini wakati Nooij akicheza mechi yake ya 15 juzi na kufungwa sita, kutoka sare sita na kushinda mechi tatu tu tangu Aprili mwaka jana alipoanza kazi, Malinzi anasema licha ya matokeo hayo, haoni sababu ya kumfukuza Mholanzi huyo. Katika mahojiano na gazeti hili jana, Malinzi alisema kwa upande wake anaona kuwa bado kocha huyo anatakiwa kupewa nafasi kwa kuwa bado sio kosa lake moja kwa moja.
Malinzi alisema akiwa Rais anatambua kuwa Watanzania wengi wamekatishwa tamaa na matokeo hayo, lakini kwa upande wake anaiona kuwa bado hiyo ni timu nzuri huku kocha wake akitakiwa kuendelea kupewa muda zaidi.
Alisema kuwa kama kukiwa na utaratibu wa kufukuza makocha hivyo itasababisha kuiharibu timu kwa kuwa sio suala la kubadili kocha ila ni kuangalia mengi zaidi.
Rais huyo aliyemfukuza Kim Poulsen na kumwajiri Nooij miezi michache baada ya kushinda urais wa TFF, alisema timu zilizoifunga Taifa Stars katika Cosafa, sio timu za kawaida ila zimejiandaa na kushiriki michuano hiyo na pia zilikuwa na michuano mingine mikubwa ambayo imetoka kushiriki.
“Mimi ninaona kuwa sio vyema kusema kuwa eti hata Madagascar imetufunga au hata Swaziland imetufunga, hiyo sio vyema kabisa kwa kuwa Swaziland imeshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika na imefanya vyema tu, na Madagascar ina makocha zaidi ya 1,000 wanatambuliwa na Fifa sasa sisi hapa hata 100 tu hawajafika,” alieleza Malinzi.
Aliongeza kuwa “kwa kuwa na makocha wengi ina maana kuwa hata timu za kawaida za mitaani zinafundishwa na watu wenye uwezo sasa hapo nataka kumaanisha kuwa sisi tungekuwa na mafanikio hayo leo tungekuwa mbali.”
Malinzi alifikia hatua ya kusema kuwa inatakiwa kuangaliwa zaidi wachezaji labda siku hiyo hawakula chakula au walikuwa hawajapewa posho au pengine viatu vilikuwa vimechakaa na ndio maana wakafungwa.
Aliongeza kuwa Kamati yaUtendaji inakutana keshokutwa kujadili masuala mbalimbali yahusuyo timu hiyo na kuongeza kuwa hakuna sababu ya kulaumiana kwa sasa ila wasubiri Kamati ikikutana ndio majibu yatafahamika.
Alisema Watanzania wanatakiwa kumuunga mkono kocha huyo kwa kuwa uwezo anao na amefundisha timu nyingi ambazo zimekuwa zikifanya vyema hadi sasa.
“Ninafahamu rekodi yake huyu sio kocha wa mchezo kwa kuwa anaweza mengi na sikukurupuka kumtafuta ila nilikuwa najua historia yake kuanzia ameshinda michezo mingapi na sare ngapi na kwetu hapa tuendelee kumpa muda,” alisema Malinzi akimzungumzia kocha huyo mwenye mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza baada ya mechi ya juzi, Nooij aliyeiwezesha Msumbiji kucheza fainali za Afcon mwaka 2012, alisema amesikitishwa na matokeo hayo, kwamba hakutegemea kupoteza mchezo dhidi ya Madagascar.
“Timu yangu haikucheza vizuri, haikuweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga huku wapinzani wetu wakitumia nafasi mbili walizozipata kupata mabao mawili katika mchezo huo,” alisema Nooij.
Stars inatarajiwa kurejea nyumbani leo usiku baada ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya Lesotho utakochezwa jioni
Comments
Post a Comment