Skip to main content

Mgombea Urais Chadema Kupatikana Agosti

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatarajia kumpata mgombea wake wa urais Agosti 4, mwaka huu.

Kupatikana kwa mgombea huyo kutatokana na uamuzi wa mkutano mkuu wa taifa, ambacho ndio chombo cha juu cha uamuzi.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kwa siku mbili.

Alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili ratiba ya kuwapata wagombea wa udiwani, ubunge na urais ambao utaratibu wa kuwapata utaanza Mei 18 hadi Agosti 4.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa ngazi ya udiwani utaanza Mei 28 hadi Juni 25.

“Julai Mosi hadi 10 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu kwa kata ambazo tuna madiwani na Julai 15 hadi 20 utakuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani wa kata pamoja na wale wa viti maalumu.

“Mei 18, hadi Juni 25 itakuwa ni kuchukua na kurejesha fomu za ubunge kwa majimbo ambayo hatuna wabunge kwa sasa pamoja na viti maalumu, na Julai 6 hadi 10 ni uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge kwa majimbo ambayo tuna wabunge kwa sasa.

“… Julai 20 hadi 25 ni uteuzi wa awali kwa wagombea ubunge kazi itakayofanywa na Kamati tendaji za majimbo. Hata hivyo pia Julai 20 hadi 25 ni kuchukua na kurejesha fomu za mgombea urais ambazo zitasimamiwa na Makao Makuu,” ilionyesha ratiba hiyo iliyotolewa na Chadema.

Pamoja na mchakato huo, Chadema imesema kuwa uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge utafanyika Agosti 1-2 kazi ambayo itafanywa na Kamati Kuu ya chama hicho.

“Agosti 3, mwaka huu kitaketi kikao cha Baraza Kuu chini ya utaratibu wa Kamati Kuu na Agosti 4 utafanyika Mkutano Mkuu wa Taifa ambao utafanya kazi ya kuchagua mgombea urais kwa mujibu wa Katiba ya Chadema,” alisema Mbowe.

Akizungumzia kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu, Mbowe alisema wamepokea, kujadili na kukubaliana makubalino yaliyokwishafikiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa – umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana ukiwa ni kikundi shinikizi katika mchakato wa Katiba katika siku za mwanzo za Bunge Maalumu la Katiba, inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema wamebaini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Serikali hawana dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya kutosha yakiwamo matakwa ya kisheria, kitaalamu na kibajeti ili kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa Katiba.

Kuhusu kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema baada ya kujadili kwa kina wamebaini kuna haja kura hiyo isogezwe mbele hadi baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu uwapo wa Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema kimsingi Chadema imebaini kutokuwapo kwa maandalizi ya vifaa, fedha, kutangaza majimbo, kata mpya pamoja na vituo.

“Kamati Kuu imeazimia kuiomba Serikali kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika Oktoba kwa mujibu wa Katiba na Serikali ya CCM isijiandae kutumia kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi sio jambo la dharura bali limekuwa likijulikana tangu miaka mitano iliyopita,” alisema.

Wakati Chadema wakitangaza ratiba yao ya kuwapata wagombea katika majimbo, vyama wenza vinavyounda Ukawa vya CUF na NCCR-Mageuzi vilishatangaza ratiba zao, lakini hadi sasa vimekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa ndani wa kuwapata wagombea wao.

Comments

Popular posts from this blog

Rais Wa Burundu "Apinduliwa"......Ndege Yake Jana Ilishindwa Kutua Burundi na Kuamua Kurudi Tanzania

Nchini Burundi, aliyekua mkuu wa majeshi Jenerali Godefroid Niyombare ametangaza Jumatano Mei 13 kuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza amepinduliwa madarakani. Meja Generali Niyombareh alisema wamechukua hatua hiyo baada ya watu wa Burundi kukataa kwa kinywa kipana awamu ya tatu ya urais wa Nkurunziza. Jenerali huyo aliyetimuliwa na Nkurunziza mwezi februari alisema kuwa Nkurunziza alishindwa kuheshimu mwafaka wa amani mbali na sheria za kimataifa. Wakati  Mapinduzi  hayo  yakitangazwa, Rais Nkurunziza alikuwa  nchini Tanzania kujumuika na viongozi wa kanda  ya Afrika Mashariki kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi tangu Nkurunzinza atangaze nia yake ya kuwania awamu ya tatu. Baada  ya  tangazo  la  kupindulikwa  kwake, Rais  huyo  alipanda  ndege  kurejea  nchini  kwake  licha  ya  tangazo  la  kufungwa  kwa  mipaka  yote  na  viwanja  vya...

Diamond Amuita Jokate Makombo...."Mwacheni Ali Kiba Ajilie Makombo"

Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amemuita mpenzi wake wa zamani Jokate Mwegelo kuwa ni makombo na kudai kama zilipendwa huyo anatembea na hasimu wake Ali Kiba, hakuna jipya kwani anakula makombo. Diamond ametoa kauli hiyo Jumatano iliyopita wakati mwanahabari wetu alipotaka kujua anajisikiaje kuona wapenzi wake wa zamani Jokate na Wema Sepetu ‘Madam’ wanamuunga mkono Ali Kiba. Pamoja na kudaiwa kuwa Jokate ana uhusiano wa ‘kimalovee’ na Ali Kiba na mwenyewe kutokubali, ameungana na Wema kuendesha kampeni ya nguvu kwenye mitandao ya kijamii kuhamasisha watu wampigie kura Kiba kwenye Tuzo za Kili 2015 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kampeni ya kuuangusha ufalme wa Diamond kimuziki. Baada ya mwanahabari wetu kuujua ‘mchezo huo’ uliopamba moto kama moto wa kifuu mitandaoni ndipo alipomuuliza Diamond anauzungumziaje ambapo kwanza alikiri kuufahamu na kudai ameudharau maana hauna jipya. “Hamna jipya waache waendelee kumpigia...

Gharama za kupima ardhi kupunguzwa

SERIKALI imesema katika mwaka ujao wa fedha itapunguza gharama za upimaji ardhi kwa zaidi ya nusu ili kuwawezesha wanachi kupima maeneo yao, hali ambayo inaonekana itapunguza migogoro ya ardhi. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara mkoani hapa kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imedumu kwa miaka mingi. Akizungumza na watendaji wa sekta mbalimbali wa mkoa wa Tabora, Waziri Lukuvi alisema Wizara itapunguza kwa zaidi ya nusu, gharama za upimaji ardhi ili kila mwananchi aweze kupima eneo lake na kupata hati ya umiliki. Lukuvi aliongeza kuwa serikali pia itaweza kukusanya kwa wingi kodi ya pango la ardhi, hivyo kuongeza mapato ambayo yataisaidia serikali katika kufanikisha shughuli za maendeleo. Pamoja na kupunguza gharama hizo, Lukuvi aliwaonya maofisa ardhi kuacha tabia ya kuendesha shughuli za serikali kwa kukiuka taratibu, akitolea mfano wa maofisa hao kupima viwanja juu ya viwanja suala ambalo limekuwa lina...