MGOMO wa mabasi ulioibuka jana, umeitikisa nchi kiasi cha kusimamisha shughuli nyingi na kusababisha adha kwa wadau katika sekta nzima ya usafirishaji.
Mbali ya abiria waliokuwa wasafiri ndani na nje ya nchi kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo na kwingineko nchini, wanafunzi wa Kidato cha Sita walioanza mitihani yao jana, baadhi yao waliathirika kwa kushindwa kufika kwa wakati katika vituo vyao vya mitihani.
Aidha, abiria katika Kituo cha Ubungo, wakionekana kukata tamaa huku muda mwingi wakinyeshewa na mvua kituoni hapo ambako hakuna sehemu za kutosha za kupumzikia abiria, walijikuta wakivamia Kituo Kidogo cha Polisi na kuanza kufanya fujo, wakitaka waonyeshwe mahali pa kula na kulala.
Abiria wengine walitoka nje ya kituo na kwenda kufunga barabara ya Morogoro, hali iliyowalazimu askari wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu kiasi, ikiwa ni pamoja na kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya.
Hali ilivyokuwa Ubungo
Katika Kituo Kikuu cha Ubungo, licha ya abiria kumiminika tangu alfajiri, wengine wakiwa na tiketi mikononi mwao, hawakuweza kusafiri kwani madereva na wasaidizi wao hawakuonekana, huku mabasi yakiwa yameegeshwa kituoni hapo.
Kituo cha mabasi Ubungo kinatumiwa na zaidi ya mabasi 600 kwa siku. Abiria walijikuta katika wakati mgumu huku mvua ikinyesha bila ya kujua hatma ya safari zao huku wengi wao wakiwa na tiketi wakiwa wamekaa ndani ya mabasi wakionekana kukata tamaa ya kusafiri.
Wakati abiria wakitafakari juu ya hatima ya safari zao, madereva wa mabasi, daladala na malori walikusanyika Ubungo kupanga mambo yao na pia kuchangishana fedha ambazo hazikuelewa zilikuwa za nini.
Miongoni mwao, huku wakiwakacha wanahabari na kuwataka waondoke eneo hilo, walibeba mabango yaliyokuwa yameandikwa, “Tanzania Bila Mgomo wa Madereva Inawezekana, Tunahitaji Mikataba Bora ya Kazi.”
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi katika ofisi za kukatia tiketi kituoni hapo waliendelea kuwahamasisha abiria kuendelea kukata tiketi wakiamini suala hilo litafikia tamati, hasa baada ya kuelezwa mambo yatakwisha baada ya mkutano wa viongozi wa madereva na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ofisini kwake.
Lakini tofauti na matarajio ya wengi, gazeti hili lilidokezwa kuwa, mkutano huo haukufanyika kwa kile kinachoelezwa baadhi ya madereva waliwadhibiti viongozi wao wasionane na Waziri Mkuu, wakishinikiza aende kuzungumza na madereva wote Ubungo.
Awali, katika eneo la kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania, Rashid Saleh alisema ni kweli kuwa wamepokea taarifa ya viongozi wa madereva kwenda kuonana na Waziri Mkuu na kwa muda huo (saa 6:30 mchana) walikuwa wakijipanga.
Alisema taarifa hiyo waliipokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na kwamba watakwenda ili kupeleka madai yao na kama hayatofanyiwa kazi kama wanavyotaka watazidi kupumzika.
“Kwa leo hadi muda huu saa sita tumewaambia madereva waende wakapumzike kwa kuwa tutawapa majibu jioni baada ya kuonana na Waziri Mkuu,” alisema Rashid.
Kutokana na mgomo huo hakuna basi hata moja lililoondoka wala kuingia kituoni hapo. Aliongeza kuwa wana matatizo makubwa na waajiri wao kuhusu suala la mikataba na kuitaka serikali kuwabana waajiri ili waweze kupata mikataba iliyo bora.
Awali, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga, alifika kituoni hapo saa 3 asubuhi na kuingia ndani ya kituo kidogo cha Polisi akionekana kujadiliana na askari Polisi waliokuwa kituoni hapo kisha kuondoka na kudai kuwa hawezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa mambo bado magumu na kwamba Waziri Mkuu atafika kituoni hapo majira ya saa sita mchana.
Muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Mpinga, mmoja wa askari aliyefahamika kwa jina la Solomon Mwangamilo aliingia ndani ya basi la Master City, huku likiwa na abiria aliliendesha hadi nje ya kituo cha mabasi, karibu na mataa ya Ubungo kwa lengo la kumshinikiza dereva aendelee na safari yake.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa dereva wa basi hilo alitokomea kusikojulikana akiogopa kuonekana msaliti kwa wenzake, jambo lililomlazimu Solomon kurejesha basi hilo ndani ya kituo.
Adha kama hizo hazikuwakuta abiria wa mabasi ya mikoani tu, bali hata watumiaji wa daladala waliojikuta wakitembea kwa miguu kwa umbali mrefu, kwani hakukuwa na usafiri, na wachache waliobahatika kupata bodaboda au magari ya mizigo aina ya Suzuki Carry maarufu kama `Kirikuu’, walitozwa nauli za juu.
Kwa ujumla, katika siku ya jana magari ya Kirikuu ndiyo yaliyotamba kwa kusafirisha abiria, sawa na bodaboda. Inaelezwa kwa magari binafsi, nauli ya chini ilikuwa Sh 2,000 ilhali kwa usafiri wa daladala, nauli ni kati ya Sh 400 na 500, ikitegemea umbali.
Kwa wanafunzi, hutozwa Sh 200, lakini jana wote walilipishwa sawa na watu wazima. Hali hiyo imeelezwa kuathiri baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita walioanza mitihani yao jana.Takribani watahiniwa 40,758 walianza mtihani yao ya mwisho ya kuhitimu Kidato cha Sita.
Serikali kusaidia Kidato 6
Kutokana na adha hiyo, Serikali imesema itaweka utaratibu maalumu wa kufanya mitihani kwa watahiniwa watakaokuwa wamechelewa mitihani ya asubuhi kutokana na mgomo wa mabasi ya abiria.
Hayo yamesemwa na Waziri mwenye dhamana ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Akizungumza wakati wa mahojiano kupitia kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na kituo cha Redio ya Taifa cha TBC Taifa, Dk Kawambwa alisema kama kutakuwepo na taarifa ya wanafunzi kushindwa kufanya mitihani yao kutokana na mgomo wa usafiri, wataweka utaratibu wa wanafunzi hao kufanya mitihani hiyo waliyoikosa.
“Tunajua kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wako bweni wengine wa kutwa, na tukipokea taarifa kutoka kwa wasimamizi wa vituo kuwa wanafunzi wamechelewa kufanya mitihani na tutaangalia sababu na kama imetokana na mgomo wa usafiri basi tutawawekea utaratibu wa kuifanya hiyo waliyoikosa,” alisema.
Jana asubuhi, watahiniwa hao walitakiwa kufanya mtihani ya Hisabati na Kiswahili na mchana walitakiwa kufanya Mtihani wa Maarifa. Aidha, akizungumza na HabariLeo jana, Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), John Nchimbi alisema mtihani umeanza vizuri maeneo mengi.
“Tumefanya ukaguzi katika baadhi ya shule, na hali ni shwari. Wanafunzi wanafanya mitihani yao katika hali ya amani na utulivu,” alisema.
Mtihani huo ambao umeanza jana na kufikia tamati yake Mei 27, mwaka huu, jumla ya watahiniwa 40,758 wamefanya mtihani wao ambapo watahiniwa wa shule ni 35,385 na wa kujitegemea ni watahiniwa 5,373.
Alipoulizwa kama wamepokea malalamiko yoyote ya wanafunzi kuchelewa mtihani wao kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria, Nchimbi alisema, “Mpaka sasa hatujapokea malalamiko yoyote kama kuna wanafunzi wameshindwa kufanya mtihani kutokana na tatizo la usafiri, ila tunafuatilia taarifa kutoka kwa wasimamizi wa mitihani ambao ni Kamati za Mitihani.”
Ingawa ofisa huyo hakuwa na taarifa za wanafunzi kuathirika, gazeti hili lilifanikiwa kupita katika shule kadhaa na kubaini mgomo huo ulivyoathiri wanafunzi.
Katika shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani, Mkuu wa Shule hiyo, Gerabline Mwanisenga alisema anashukuru wanafunzi wa shule yake wamewahi kufika na kuanza mtihani kwa wakati japokuwa walipata shida ya usafiri.
“Tulipata wasiwasi sana kama wanafunzi wangeweza kuwahi kwenye chumba cha mtihani, lakini nashukuru hakuna hata mmoja ambaye amechelewa japokuwa wamehangaika sana na wengine imewalazimu kukimbia kwa umbali mrefu ili waweze kuwahi,” alisema Mwanisenga.
Katika shule nyingine, hali ilikuwa hivyo, na baadhi ya wanafunzi walielezea kuathirika na mgomo huo kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya nauli, na hivyo kukataliwa na kulazimika ama kutembea au kudandia lifti.
Mbeya, Arusha ni mateso
Hali ya ugumu wa usafiri imeripotiwa kutokea katika mikoa mbalimbali nchini, ikiweno Mbeya na Arusha ambako mamia ya abiria walilazimika kutembea kwa miguu kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na mgomo huo.
Jijini Mbeya, abiria wa kwenda mikoani walikwama kutokana na mabasi kutofanya safari na hakuna hata basi moja lililotoka katika kituo kikuu cha mabasi jijini hapa kuanza safari.
Kwa abiria wa safari za ndani ya Jiji, mbali na kutembea kwa miguu baadhi yao walilazimika kukodi pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda na zile za miguu mitatu maarufu kama bajaji ili kuweza kuwahi kazini na maeneo ya biashara jambo lililopelekea kupata usumbufu mkubwa.
Hata hivyo baadhi ya madereva na makondakta wa daladala jijini Mbeya walionekana kutofurahishwa na kitendo cha pikipiki hizo kutoa huduma ya kusafirisha abiria.
Hali kama hiyo imeripotiwa pia jijini Arusha ambako magari binafsi na bodaboda ndiyo yaliyogeuka wakombozi, lakini yakitoza nauli kubwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii eneo la Stendi Kuuu ya Mabasi mkoani Arusha, dereva wa basi la Saibaba, Gideon Ngumuo alisema madereva wanalazimisha mikataba kwa kuwa wanaishi maisha magumu, akitolea mfano kuwa dereva anakuwa na Mkataba wa mwaka mmoja huku akilipwa Sh 200,000 kwa mwezi na posho ya Sh 13,000 kila siku anaposafiri , kiasi hicho kikihusisha chakula na fedha ya kuachia familia.
“Tunahitaji mikataba ya kudumu ya ajira kwa madereva wa mabasi nchi nzima chanzo cha ajali ni kingi misongo ya mawazo inatusumbua hivi kweli posho hiyo inaweza kuendesha familia utaacha nyumbani shilingi ngapi na watoto watakula nini sasa tukigoma wanasema tunagomea kusoma… lakini hiki ndicho kitu kinachotufanya tugome, tumechoka na mkitulazimisha kuondoa magari bila kutuambia muafaka ni upi basi tutaendelea kusikia ajali ajali,” alisema.
37 mbaroni kwa`Hiace’ lenye mawe
Kutoka mkoani Dodoma, Sifa Lubasi anaripoti kuwa, Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu 37 waliokuwa maeneo la Chaduru na Nkuhungu mjini Dodoma wakiwa na mawe na kuwazuia madereva ambao walikuwa wanatoa huduma za usafiri kwa abiria baada ya madereva wa mabasi makubwa ya abiria na daladala kugoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime alisema watu waliokamatwa ambao wengi wao ni vijana hawahusiani na udereva wa basi au daladala walikuwa wakitumia Hiace mbili ambazo namba zake ni T.936 AVU na T.704CVG kuzunguka kwa lengo la kuwazuia walioamua kubeba abiria.
“Walichokuwa wakifanya ni kuzuia magari yasipakie abiria na kuwakataza kupita katika maeneo hayo hata yale magari binafsi wasibebe yeyote hata kama wanafanya kazi ofisi moja au ni jirani yake,” alisema.
Alisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kutokana na ukiukaji huo wa sheria, watafikishwa mahakamani. Pia alisema madereva wa mabasi baadaye walianza safari za kuelekea mikoa mbalimbali na hali ni shwari.
Awali, vikosi vya Jeshi la Polisi vililazimika kusindikiza mabasi ya Kampuni ya Shabiby ambayo jana hayakujihusisha na mgomo wa wamiliki na madereva wa mabasi.
Inaelezwa kuwa, awali kulikuwa na taarifa ya kundi la wahalifu kutaka kuvamia mabasi yanayofanya safari katika maeneo mbalimbali ya njia kuu zinazounganisha mkoa wa Dodoma na mingine nchini.
Madereva Rukwa wapuuza mgomo LICHA ya madereva wa mabasi katika mikoa mbalimbali nchini kugoma kufanya kazi jana, hali ni tofauti mkoani Rukwa ambako waliendelea kutoa huduma kwa wasafiri kama kawaida.
Mwandishi wa gazeti hili alifika Stendi Kuu ya Sumbawanga alfajiri ya jana na kushuhudia mabasi yanayofanya safari za mikoa ya Mbeya na Ruvuma yakiendelea na ratiba zake kama kawaida.
Wakizungumza kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini baadhi ya madereva hao wamedai kuwa hawaoni sababu za msingi kugoma huku baadhi yao wakikiri kuwa hawafahamu lolote kuhusiana na mgomo huo.
“Waache wagome sisi tunaendelea na kazi kama kawaida mie siko tayari kupoteza kazi yangu kwa kuwa tajiri yangu ametutishia kuwa yeyote anayedai mkataba akatafute kazi pahala pengine …….sasa baadhi yetu tumebeba majukumu makubwa ya kifamilia hatuna pa kukimbilia,“ alisema mmoja wao.
Kwa upande wa wakata tikiti na wapiga debe katika stendi hiyo kuu ya mabasi yanayofanya safari ndani na nje ya mkoa huo wamewapongeza madereva hao kutounga wenzao mkono wakidai kazi hiyo ndio inayowapatia riziki.
“Isitoshe sisi tuko huku pembezoni hatuhusiani kabisa na hao wa hiyo mikoa mingine hata kimapato ...tunawapongeza madereva wa mkoa huu kwa msimamo wao huo vinginevyo tungekufa njaa,” anasema mkatisha tikiti.
Hata hivyo baadhi ya wasafiri ambao wanalazimika kufika Mbeya ili waweze siku inayofuata kuendelea na safari hadi mikoa mingine ikiwemo Dar es Salaam walieleza wasiwasi wao kutokana na taarifa ya madereva wa miji mingi nchini kuanza mgomo wao leo.
“Nasafiri lakini bado nina mashaka makubwa kwani nakwenda Dar sasa zipo taarifa kuwa madereva wa miji mingi nchini wameanza mgomo hivyo ukiendelea ina maana nitasota Mbeya ….. hata hivyo itajulikana huko huko mbele ya safari,“ anasema John Mwakipesile aliyekuwa anasafiri kwenda Dar kupitia Mbeya.
Waziri Mkuu aunda Kamati Wakati hayo yakitokea, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati ya Kudumu ya kusimamia usafiri wa barabarani nchini, kwa lengo la kuhakikisha kwamba kunakuwa na majadiliano shirikishi ya wadau wote ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya makundi mbalimbali katika usafiri wa barabarani bila kusubiri mgomo.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kuhusu mgomo wa madereva unaohusisha mivutano kati yao na waajiri pamoja na SUMATRA, TABOA na TATOA.
“Mara kadhaa imetokea kwamba wahusika wanatumia njia za migomo kufanya shinikizo ili madai yao yatimizwe. Hali hii imesababisha usumbufu mkubwa kwa jamii hususani katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo usafiri wa watu wengi unategemea mabasi madogo ya daladala,” alisema.
Aidha alisema kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo ambacho ni eneo muhimu kwa usafiri wa kwenda mikoani nacho huathiriwa sana na migomo hiyo.
“Baada ya kutafakari hali hii, imebainika kwamba kwa kuwa madai haya yanahusu taasisi mbalimbali na pia yanagusa sheria mtambuka, yamefanyika mashauriano ndani ya serikali ambapo juzi Mei 2, Waziri Mkuu ameunda kamati hiyo,” alisema.
Alisema; “ni maoni ya serikali kwamba kutokuwa na Kamati ya Kudumu ya Kusimamia changamoto mbalimbali katika usafiri wa barabarani kumechangia sana kukosekana kwa mashauriano baina ya wadau ili kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali kila yanapotokea.”
Alisema wanaounda kamati hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ambaye ni Mwenyekiti kwa ajili ya kusimamia Sera ya uchukuzi, Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni Mjumbe na anawakilisha usimamizi wa polisi na usalama barabarani na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira ambaye anasimamia masuala ya mikataba ya ajira kati ya TATOA/TABOA na madereva.
Wajumbe wengine ni Katibu Mkuu Ujenzi kwa ajili ya masuala ya barabarani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya masuala ya sheria. Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Uratibu wa Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa TABOA na Mwenyekiti wa TATOA.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi na Magari ya Mizigo, Mwenyekiti wa Chombo cha Kusimamia Haki za Wasafiri, Kamishna wa Polisi, Usalama Barabarani na Mkurugenzi wa SUMATRA.
Alisema Waziri Mkuu ameagiza kamati hiyo ikutane mara moja na kazi yake ya kwanza iwe ni kufanya uchambuzi wa matatizo yaliyolalamikiwa na wadau mbalimbali na pia ichambue kiini cha kutokutekelezwa kwa makubaliano ya msingi yaliyokwishafikiwa.
“Kwa yale mambo yaliyoshindikana hadi sasa na yanayohitaji mabadiliko ya sheria na kanuni, Kamati ipendekeze kwenye ngazi za juu ili ufumbuzi upatikane.”
Alisema ni matumaini ya serikali kuwa kwa utaratibu huo mpya hakutakuwa na ulazima wa mdau yeyote kusitisha huduma kwa umma jambo ambalo linaleta adha kubwa na isiyostahili kwa jamii.
Aliwataka wahusika kuwa wastaarabu na kukaa mezani na kusisitiza kwamba hawategemei mgomo tena baada ya majadiliano hayo kwa kuwa kufanya mgomo ni kuwaadhibu wananchi.
“Kwa kawaida hauwezi kufanya mkutano wa hadhara Ubungo ukasema unatatua mgomo bali mgomo utatatuliwa kwa kukaa mezani na kujadiliana…serikali haivumilii hata kidogo mateja na wapiga debe kuzuia usafiri,” alisema.
Alitoa mwito kwa polisi kuchukua hatua kali kwa watu wa aina hiyo wakiwemo madereva wanaozuia wenzao wasiendeshe magari kwa kuwa uhuru unatakiwa kuzingatia haki za wengine.
“Hatuwezi kuvumilia jamii ya Watanzania ambayo inataka kuweka rehani maisha ya wengine. Tutachukua hatua kwa wakaidi ikiwemo, kuwanyang’anya leseni… Uvumilivu wa serikali una mwisho, hatuwezi kuendelea kuvumilia,” alisema.
Chanzo cha mgomo
Madereva hao wamegoma wakidai haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa hatua ya kusoma kila baada ya leseni kuisha, mikataba bora, posho za safari na mishara inayokidhi malipo na bima kwa dereva.
Hii ni mara ya pili kwa madereva hao kufanya mgomo, kwani Aprili 10, mwaka huu, waligoma na kusababisha adha kubwa ikiwa ni pamoja na kuyumbisha shughuli za kiuchumi na kijamii karibu nchi nzima.
Lucy Lyatuu, Anastazia Anyimike, Hellen Mlacky na Emmanuel Ghula (Dar), Sifa Lubasi (Dodoma), Veronica Mheta (Arusha), Peti Siyame (Sumbawanga) naJoachim
Comments
Post a Comment