WASANII wametakiwa kuwa wabunifu zaidi katika sanaa ili kutengeneza kazi nzuri zenye kutoa elimu mahususi pamoja na burudani kwa jamii.
Hayo yalisemwa mwanzoni mwa wiki hii na msanii mkongwe wa sanaa za maonesho pamoja na maigizo nchini, Bakari Mbelemba maarufu Mzee Jangala alipozungumza na mwandishi wa habari hii.
Mzee Jangala aliyejizolea umaarufu kwenye michezo ya kuigiza iliyokuwa ikirushwa na kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) wakati huo (sasa TBC Taifa) alisema wasanii wanatakiwa kuisoma sanaa zaidi ili watengeneze kazi nzuri.
“Sanaa ina pesa ila tatizo ni kwamba wasanii wenyewe wanashindwa kwenda shule kusoma sanaa pamoja na kutumia ubunifu ili kutengeneza kazi nzuri zinazoelimisha jamii,” alisema Jangala.
“Ili mtu afanye kazi vizuri kwa ufasaha ni lazima apate elimu ya kutosha hivyo hata wasanii tunapaswa kwenda shule ili kujifunza sanaa kwani mbolea ya sanaa ni elimu,” alisema.
Licha ya sanaa kuwa ajira kwa vijana wengi, wasanii wengi wamekuwa wakiifanya kazi hiyo kwa kutumia vipaji zaidi badala ya kwenda shule, hali inayofanya kazi zao kuwa na kiwango cha chini
Comments
Post a Comment