Published on Wednesday, 27 May 2015 00:29
Written by Khatib Suleiman, Zanzibar
Hits: 72
SERIKALI ya Oman imeikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hundi ya Sh bil 12.3 kwa ajili ya kiwanda cha uchapishaji, pamoja na nyaraka za magari 10 ya msaada, yaliyotolewa yatumiwe na viongozi.
Wakati akikabidhi hundi na nyaraka hizo kwa Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein, Ikulu mjini hapa jana, Balozi wa Oman nchini, Saoud Ali Mohamed Al Ruqaishi alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kununua mashine za kuchapisha magazeti na vitabu.
Akitoa shukrani, Dk Shein aliipongeza Serikali ya Oman.
Alisema, msaada huo utaiwezesha Serikali yake kufikia malengo ya kuwa na kiwanda cha kisasa cha upigaji chapa, na kwamba, hautatumika kwa malengo tofauti.
Alisema, “Msaada huu unathibitisha ushirikiano mzuri wa muda mrefu kati ya Serikali hizi mbili”.
Inaelezwa kuwa, Serikali ya Oman imekwisha toa misaada mingi kwa Zanzibar, ikiwemo kujenga Chuo cha Afya kilichopo Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Balozi huyo alisema, uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili utadumishwa.
Comments
Post a Comment