Skip to main content

Sekta ya elimu inavyojielekeza Dira 2025

DIRA ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa 2011/12 hadi 2024/25, vinaonesha kwamba Sekta ya Elimu na Mafunzo, ndio inayotarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu.

Maendeleo hayo ni katika kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia lengo hili, mfumo wa elimu na mafunzo unaotumika nchini lazima utoe fursa za kutosha kwa watu kujielimisha.

Katika kufanikisha hili, Serikali imekuwa ikitekeleza sera mbalimbali kuanzia Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996), Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu Msingi (2007) ambazo zimekuwa na mafanikio mbalimbali.

Sera hizo za elimu, kwa ujumla, zilitoa mwongozo kuhusu kuongeza ushirikishwaji wa sekta binafsi; kuongeza fursa za elimu na mafunzo kwa usawa na kupanua wigo wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome anasema katika miaka 19 ya utekelezaji wa Sera ya kwanza ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 pamoja na sera nyingine mahususi za elimu na mafunzo, Tanzania imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu.

“Mafanikio haya ni pamoja na kupanua wigo wa elimu katika ngazi zote, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu,” anasema Profesa Mchome. Anasema idadi wa watoto wanaojiunga na elimu ya awali imeongezeka kutoka asilimia 24.7 mwaka 2004 hadi 37.3 mwaka 2013 na kiwango cha watoto walioandikishwa katika elimu ya msingi imeongezeka kutoka asilimia 77.6 mwaka 1995 hadi asilimia 96.2 mwaka 2013.

Aidha kiwango cha watoto wanaojiunga na elimu ya sekondari kimeongezeka pia kutoka asilimia 14.6 mwaka 1995 hadi 59.5 mwaka 2013. Hali kadhalika, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi imeongezeka kutoka 4,641 mwaka 2000/01 hadi 145,511 mwaka 2012/13.

Anasema elimu ya juu imepanuka ambapo vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vimeongezeka kutoka chuo kimoja mwaka 1995 hadi 50 mwaka 2013 na kuwezesha idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu kwa ngazi ya Shahada kuongezeka kutoka 16,727 mwaka 2000/01 hadi 162,510 mwaka 2012/13.

Utekelezaji wa Sera za Elimu na Mafunzo ya Ufundi ulifanyika kupitia sheria, kanuni, miongozo pamoja na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu iliyoandaliwa mwaka 1997. Pia kulikuwa na mipango na programu mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Ugatuaji wa majukumu katika sekta ya elimu na mafunzo umefanyika kutoka Serikali Kuu kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa, vyombo vya ithibati na uthibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi, elimu ya vyuo vikuu, mfuko wa elimu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu pia vimeanzishwa na vinafanya kazi nzuri ya kuendeleza elimu na mafunzo nchini.

Hata hivyo, Waziri wa Wizara hiyo, Shukuru Kawambwa anasema, changamoto nyingi zimejitokeza katika kipindi cha utekelezaji wa Sera hizi, ambazo zimekuwa zikiathiri ubora na usawa katika elimu inayotolewa kwenye ngazi mbalimbali. Changamoto hizi ni pamoja na upungufu wa miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vitabu, maabara, maktaba na madarasa.

Anataja changamoto nyingine ya elimu kuwa ni utekelezaji wa sera za elimu na mafunzo kukosa mfumo nyumbufu unaoruhusu elimu na mafunzo kupatikana na kutambulika kwa njia mbalimbali mbadala.

“Changamoto nyingine ni kuwepo kwa elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora visivyotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa, kutokuwa na mfumo wa ajira unaowezesha upatikanaji wa wataalamu wa kada mbalimbali wanaohitajika katika sekta ya elimu na mafunzo nchini,” anasema Kawambwa.

Kawambwa anasema tangu kuanza kutekelezwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia ambayo yameleta changamoto na kuzifanya sera hizo zipitwe na wakati.

Mabadiliko ya kiuchumi duniani anasema yameleta msukumo kwa nchi zinazoendelea na zilizoendelea ama kubadilisha au kuimarisha sera, programu na mikakati yake ili ziweze kuhimili ushindani wa kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii, kisayansi na kiteknolojia.

Anasema kukua huku kunatokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Azma ya Tanzania ni kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo sekta ya elimu na mafunzo imepewa jukumu la kuandaa rasilimaliwatu ya kutosha kwa ajili ya kukidhi mabadiliko hayo.

Majukumu ya Wizara anayataja kuwa ni kuutunga Sera ya Elimu na Mafunzo katika ngazi zote, kuweka na kusimamia viwango vya ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, kuweka na kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti ya maendeleo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya ufundi (ikiwemo ualimu) na elimu ya juu.

Mengine ni kufuatilia na kufanya tathmini ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya ufundi na elimu ya juu, kujenga uwezo wa idara za makao makuu, taasisi na vyombo vilivyo chini ya Wizara kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake kama yanavyoainishwa na mkakati wa utekelezaji wa sera.

Wizara pia ina jukumu la kutumia matokeo ya tathmini, utafiti na taarifa mbalimbali zinazohusu hali halisi ya utoaji wa elimu na mafunzo katika kutoa maamuzi yenye tija na yatakayoongeza ufanisi katika utekelezaji wa mkakati wa sera. Profesa Mchome anasema Serikali imekuwa ikiweka mfumo nyumbufu katika elimu na mafunzo ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kujielimisha na kuwa huru kutafuta elimu katika fani wanayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wao.

Anasema serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikiimarisha usimamizi, ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote. Pia imekuwa ikijielekeza katika kuimarisha mfumo, mbinu, dhana na falsafa ya ukaguzi wa shule ili kuleta ufanisi.

Kadhalika anasema katika kipindi chote cha kuelekea Dira ya Maendeleo 2025, Serikali, kwa kushirikiana na wadau, imekuwa na itaendelea kuhuisha mitaala iliyopo katika ngazi zote za elimu na mafunzo ili iende na wakati na kukidhi mahitaji ya elimu na mafunzo ya sasa na siku zijazo kwa kuzingatia mahitaji ya Taifa, walengwa na soko la ajira.

Profesa Mchome Serikali pia inahakikisha mitaala inazingatia stadi za msingi za mawasiliano, kusoma, kuandika na kukokotoa; kutafiti, kuchambua taarifa; kutafsiri, kutathmini na kutumia maarifa, uvumbuzi, ubunifu na ujasiriamali katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

“Serikali itaimarisha usimamiaji na upimaji wa utekelezaji wa mitaala katika taasisi za elimu na mafunzo katika ngazi zote, ili kuleta ufanisi wa elimu na mafunzo yatolewayo.

Itaimarisha muundo na utaratibu wa ufundishaji wa masomo ya Hisabati, Sayansi na Teknolojia katika ngazi zote za elimu na mafunzo,” anasema. Anasema Serikali itahakikisha matumizi zaidi ya Sayansi na Teknolojia katika utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi zote.

Pia anasema serikali itahakikisha kuwepo kwa miundombinu bora na stahiki ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote

Comments

Popular posts from this blog

Rais Wa Burundu "Apinduliwa"......Ndege Yake Jana Ilishindwa Kutua Burundi na Kuamua Kurudi Tanzania

Nchini Burundi, aliyekua mkuu wa majeshi Jenerali Godefroid Niyombare ametangaza Jumatano Mei 13 kuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza amepinduliwa madarakani. Meja Generali Niyombareh alisema wamechukua hatua hiyo baada ya watu wa Burundi kukataa kwa kinywa kipana awamu ya tatu ya urais wa Nkurunziza. Jenerali huyo aliyetimuliwa na Nkurunziza mwezi februari alisema kuwa Nkurunziza alishindwa kuheshimu mwafaka wa amani mbali na sheria za kimataifa. Wakati  Mapinduzi  hayo  yakitangazwa, Rais Nkurunziza alikuwa  nchini Tanzania kujumuika na viongozi wa kanda  ya Afrika Mashariki kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi tangu Nkurunzinza atangaze nia yake ya kuwania awamu ya tatu. Baada  ya  tangazo  la  kupindulikwa  kwake, Rais  huyo  alipanda  ndege  kurejea  nchini  kwake  licha  ya  tangazo  la  kufungwa  kwa  mipaka  yote  na  viwanja  vya...

Diamond Amuita Jokate Makombo...."Mwacheni Ali Kiba Ajilie Makombo"

Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amemuita mpenzi wake wa zamani Jokate Mwegelo kuwa ni makombo na kudai kama zilipendwa huyo anatembea na hasimu wake Ali Kiba, hakuna jipya kwani anakula makombo. Diamond ametoa kauli hiyo Jumatano iliyopita wakati mwanahabari wetu alipotaka kujua anajisikiaje kuona wapenzi wake wa zamani Jokate na Wema Sepetu ‘Madam’ wanamuunga mkono Ali Kiba. Pamoja na kudaiwa kuwa Jokate ana uhusiano wa ‘kimalovee’ na Ali Kiba na mwenyewe kutokubali, ameungana na Wema kuendesha kampeni ya nguvu kwenye mitandao ya kijamii kuhamasisha watu wampigie kura Kiba kwenye Tuzo za Kili 2015 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kampeni ya kuuangusha ufalme wa Diamond kimuziki. Baada ya mwanahabari wetu kuujua ‘mchezo huo’ uliopamba moto kama moto wa kifuu mitandaoni ndipo alipomuuliza Diamond anauzungumziaje ambapo kwanza alikiri kuufahamu na kudai ameudharau maana hauna jipya. “Hamna jipya waache waendelee kumpigia...

Gharama za kupima ardhi kupunguzwa

SERIKALI imesema katika mwaka ujao wa fedha itapunguza gharama za upimaji ardhi kwa zaidi ya nusu ili kuwawezesha wanachi kupima maeneo yao, hali ambayo inaonekana itapunguza migogoro ya ardhi. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara mkoani hapa kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imedumu kwa miaka mingi. Akizungumza na watendaji wa sekta mbalimbali wa mkoa wa Tabora, Waziri Lukuvi alisema Wizara itapunguza kwa zaidi ya nusu, gharama za upimaji ardhi ili kila mwananchi aweze kupima eneo lake na kupata hati ya umiliki. Lukuvi aliongeza kuwa serikali pia itaweza kukusanya kwa wingi kodi ya pango la ardhi, hivyo kuongeza mapato ambayo yataisaidia serikali katika kufanikisha shughuli za maendeleo. Pamoja na kupunguza gharama hizo, Lukuvi aliwaonya maofisa ardhi kuacha tabia ya kuendesha shughuli za serikali kwa kukiuka taratibu, akitolea mfano wa maofisa hao kupima viwanja juu ya viwanja suala ambalo limekuwa lina...