SERIKALI imesema baada ya kukamilisha ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa mbalimbali nchini, itashughulikia barabara za mkoa mmoja mmoja.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alisema hayo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo (CCM).
Lwenge alisema kwa sasa serikali imejikita katika kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa kwa barabara za lami, na itakapokamilisha hilo, itazigeukia barabara za mkoa mmoja mmoja ili kuziweka katika hali bora.
Awali, akijibu swali la msingi la Mitambo, alisema barabara ya Liwale-Nanguruku ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 230. Naibu Waziri alisema katika mwaka wa fedha 2012/13, barabara hiyo ilitengewa jumla ya Sh milioni 1,066.92 na katika mwaka wa 2013/14, jumla ya Sh milioni 1,782.69 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. “Aidha, kufuatia mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara ulitokea na kusababisha uharibifu mkubwa. “Kutokana na hali hii, barabara hii iliidhinishiwa jumla ya Sh milioni 1,091.53 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya dharura na kurudisha mawasiliano yaliyokuwa yamekatika katika barabara hii,” alisema Naibu Waziri
Comments
Post a Comment