MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe, amesema zoezi la kumtamfuta mrithi wa kocha Goran Kopunovic tayari limeanza na nchi ambazo wamezilenga ni Serbia, Sweden na Uingereza.
Hans Poppe alisema jana kuwa bado hawajamaliza mazungumzo na kocha wao wa sasa Kopunovic, lakini wana wasiwasi huenda wasifikie muafaka kutokana na kocha huyo kupata tamaa na kuhitaji kiasi kikubwa cha fedha tofauti na kile cha awali.
Hata hivyo habari za ndani ambazo gazeti hili inazo ni kwamba Simba imeshafanya maamuzi ya kuachana na Kopunovic baada ya kutaka kulipwa Shilingi milioni 100 kwa mkataba usiozidi mwaka mmoja.
Hans Poppe, alisema wameamua kufanya hivyo lengo ni kujiweka tayari kwa chochote kitakachotokea kuhusiana na kocha huyo kama ikishindikana kuendelea naye wawe na kazi nyepesi ya kumalizana na kocha mpya ambaye ndiyo wanamtafuta hivi sasa.
“Lengo letu ni kuanza mapema maandalizi kwa ajili ya msimu ujao pamoja na michuano ya Kombe la Kagame kwa hiyo lazima tujiandae kwa kila kitu ndiyo sababu kwa sasa tupo katika mazungumzo na makocha sita ambao mmoja wao anaweza kuifundisha timu yetu kama mazungumzo na Kopunovic yatashindikana,”alisema Hans Poppe.
Hans Poppe amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu wakati uongozi wao ukiendelea kupambana kuwaletea kocha atakaye ibadili timu yao na kuipa mafanikio makubwa msimu ujao ikiwemo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Kopunovic aliwasili nchini mwishoni mwa Desemba mwaka jana na kuingia mkataba wa miezi sita kuifundisha Simba baada ya Mzambia Patrick Phiri kutupiwa virago.
Simba iliamua kuachana na Phiri baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu. Kopunovic aliikuta Simba ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo na kuiongoza mpaka kumaliza ligi nafasi ya tatu.
Comments
Post a Comment