Nyalandu amewaonya watendaji wa wizara yake wanaojifanya miunguwatu na kushindwa kufuata taratibu za kazi na kunyanyasa wananchi, kuwa atawaondoa mchana kweupe.
Alisema ana mamlaka ya kufanya hivyo muda wowote na kwamba kila bora na makini ni yule mwadilifu na anayejali na kushughulikia matatizo ya wananchi na si kunyanyasa ama vinginevyo.
Aliwataka wananchi hususan jamii ya wafugaji kumfikishia taarifa sahihi kuhusu wahifadhi kwenye mapori ya akiba wanaowatoza faini kubwa ama kuagiza mifugo ipigwe risasi ili ashughulike nao kwani ni kinyume cha sheria.
“Hakuna mtendaji wa wizara yangu aliyepo juu ya sheria…unyanyasaji na rushwa ni makosa ya jinai na kamwe sitakubali yawepo ndani ya taasisi za wizara ninayoiongoza. Kila mtendaji afuate sheria na anayekiuka nina mamlaka ya kumuondoa muda wowote,” alisema Nyalandu wakati alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wafugaji kutoka mikoa yote nchini, uliofanyika juzi jioni mjini Lamadi mkoani Simiyu.
Kauli hiyo inatokana na wafugaji kulalamika kuonewa na baadhi ya watendaji, hususan wahifadhi na askari wa wanyamapori. Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye, alisema matukio ya wafugaji kunyanyaswa yameshika kasi na wahusika wakubwa ni wahifadhi na askari wa wanyamapori.
Alisema matukio ya ng’ombe kukamatwa na kupigwa risasi ndani na nje ya hifadhi, yamezidi kushika kasi huku watendaji wakijigamba hakuna wa kuwakataza wala kuwawajibisha kwa ukatili huo.
Kutokana na malalamiko hayo, Nyalandu amepiga marufuku wahifadhi na askari wa wanyamapori kujichukulia sheria mkononi na kuheshimu haki za wengine.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, amewaonya watendaji wanaopiga marufuku ama kukwamisha usafirishaji wa mifugo kwenda nchi ya nchi, kuacha tabia hiyo kwani wanahujumu uchumi.
Alisema mifugo inayosafirishwa nje ya nchi na ambayo imefuata taratibu, ikiwa ni pamoja na mfanyabiashara kuwa na vibali halali vya serikali, haipaswi kuzuiwa na kupiga marufuku tabia hiyo.
Amewaonya baadhi ya wafanyabiashara wanaosafirisha mifugo kwenda nje kwa kutumia njia za panya na wengine kutumia vibali vya kughushi arobaini yao imefika na wajiandae kupanda mahakamani kwa kuhujumu uchumi.
Dk Kamani alikuwa akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara, uliowakutanisha wafugaji kutoka mikoa yote nchini, uliohudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Erasto Mbwilo.
Mkutano huo ulikuwa ukifikisha kilio cha muda mrefu cha wafugaji kuhusiana na maeneo ya malisho na manyanyaso, wanayodai kufanyiwa na wahifadhi kwenye mapori ya akiba na askari wa wanyamapori.
Alisema mifugo inayosafirishwa nje ya nchi inakuza uchumi wa taifa na wafugaji kwa ujumla na kwamba, tabia za baadhi ya watendaji kukwamisha kwa sababu zao binafsi ili kupata chochote hazikubaliki.
Pia alitumia fursa hiyo kuagiza kuwa asilimia 10 ya mapato ya minada ya mifugo itengwe kwa ajili ya kuboresha sekta ya mifugo nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya malisho na maji kwa wafugaji.
Awali, katika risala yao kwa Nyalandu, wafugaji hao walilalamikia kunyanyaswa na wahifadhi, ikiwa pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi wao na mifugo wao.
Walidai kutokana na manyanyaso hayo wamegeuzwa kuwa mashine za kutolea pesa (ATM) na wahifadhi wakiwemo askari wanayamapori wanapowakamata na kuwatoza kuwatoza faini kubwa kuliko kawaida na fedha hizo huishia mifukoni mwao
Comments
Post a Comment