wanatarajiwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete mjini Arusha, wiki ijayo wakati kiongozi huyo wa nchi atakapokuwa akifungua rasmi mkutano wao mkuu wa mwaka kitaifa.
“Tunatarajia kuwa walimu wapatao 1,200 kutoka mikoa 25 na wilaya 153 za Tanzania Bara watakutana na Rais Kikwete katika eneo la Ngurdoto, wilayani Meru, mkoani Arusha.
Mkutano huo Mkuu wa Chama cha Walimu Taifa (CWT) utafanyika kati ya Mei 26 hadi 28, mwaka huu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Juvin Buruya na kuongeza: “Walimu wote Tanzania watawakilishwa vema kwenye mkutano huo ambapo tutatumia fursa ya uwepo wa Rais Kikwete kumuomba amalizie ahadi zake kadhaa alizowaahidi wakufunzi hao kabla hajastaafu rasmi,” alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa CWT mkoani Arusha, walimu watakaojumuika kwenye mkutano mkuu, watatumia fursa hiyo kumuaga rasmi mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mwalimu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema chama hicho kimekuwa kikipata ushirikiano mzuri kutoka serikali ya awamu ya nne, na kwamba wanatarajia uhusiano huo mzuri kuendelea hata katika serikali ijayo ya awamu ya tano.
Oluoch alisema nchi sita zinatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambazo ni Uganda, Kenya, Denmark, Rwanda na Ghana, ambapo pia viongozi wastaafu wa CWT taifa pamoja na wawakilishi kutoka visiwa vya Zanzibar watakuwepo.
“Malengo makuu ya mkutano mkuu wa CWT taifa ni pamoja na kujadili taarifa za kazi ya chama na taarifa za mapato na matumizi pamoja na kupitia mpango mkakati wa miaka mitano 2015-2020,” aliongeza Naibu Katibu Mkuu.
CWT pia itafanya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kitaifa Mei 28, mwaka huu na tayari wagombea wapatao 452 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za CWT.
Nafasi hizo ni pamoja na Urais wa CWT, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina wa taifa, wawakilishi wa makundi maalumu yakiwemo yale ya walimu wanawake, walimu wenye ulemavu, walimu vijana pamoja na wadhamini wa chama.
Comments
Post a Comment