YANGA imerejea jana kutoka Tunisia ilikotolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikisema ipo haja kwa Watanzania kuachana na uungwana na ukarimu kwa timu za kigeni zinazokuja kucheza nchinikutokana na mambo wanayofanyiwa timu za Tanzania ugenini.
Aidha, makocha wake wanajivunia timu yao kuonesha umahiri licha ya kucheza na timu ngumu, Etoile Sportive du Sahel.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa akizungumza na gazeti hili baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana alasiri, alisema timu yao ilicheza vizuri, lakini hali ilikuwa ngumu kipindi cha pili cha mchezo huo waliofungwa bao 1-0 kwani wenyeji, waliamua ‘kupaki’ basi.
Yanga ilifungwa bao 1-0 na kutolewa katika raundi ya pili baada ya matokeo ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 18, mwaka huu, kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
“Kama tulivyoeleza kabla ya kuondoka nchini kwamba tumejipanga kwenda kushindana. Vijana walipambana na Watanzania wamejionea wenyewe. Walicheza vizuri na kuonesha uwezo mkubwa,” alisema Mkwasa na kuongeza: “Hali ilikuwa ngumu kipindi cha pili kwa sababu licha ya vijana kuzidi kupambana kwa ku-press zaidi, wenzetu waliamua kurudi nyuma na kuwa wengi zaidi wakilinda lango lao. Hii ilitupa wakati mgumu katika kupenya na kupata bao la kusawazisha.”
Mkwasa anayemsaidia Mholanzi Hans van der Pluijm aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa uwezo mkubwa waliouonesha katika mashindano hayo mwaka huu, akisema yalikuwa magumu, lakini wameona mambo ambayo wanatakiwa kuyafanyia kazi ili mwakani wafanye vizuri zaidi.
Kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, mwakani Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, na Mkwasa anasema: “Tumeona mashindano ya mwaka huu, yapo marekebisho madogo ambayo tutayafanya, lakini tunajivunia kikosi chetu, kina vijana wadogo, lakini wameonesha uwezo mkubwa katika ligi na michuano ya kimataifa.”
Kuhusu mambo wanayokutana nayo katika mechi za ugenini, Mkwasa alisema: “Naamini wakati umefika kwa Watanzania kuacha kuwa waungwana na wakarimu kwa timu zinazokuja hapa. Wenzetu wanatumia mbinu nyingi kutuvuruga kabla ya mechi. “Kwa mfano, mnawekwa uwanja wa ndege masaa matatu, wanawaletea magari mabovu, mnapewa uwanja wa mazoezi kwa muda mfupi. Yaani yote ni kuhakikisha wanawavuruga na kushinda kirahisi. Ni lazima na sisi sasa tuwe na roho ya kikatili.”
Akizungumzia maandalizi ya mechi yao ya kesho ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Mkwasa alisema licha ya kutwaa ubingwa, wataingia uwanjani kesho wakiichukulia mechi hiyo kwa uzito mkubwa.
“Hii ni mechi ngumu, Azam FC ni timu nzuri, na juzi wameshindwa, hivyo wataongeza nguvu zaidi katika mechi yetu. Nasi tunajiandaa kwa nguvu zote, tunaichukulia mechi hii kwa umuhimu mkubwa,” alisema Mkwasa.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Bara msimu wa 2014/2015 kabla ya kwenda Tunisia kwa kufikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 13 zinazoshiriki ligi hiyo, na imebakiza mechi mbili dhidi ya Azam FC na Ndanda FC.
Kesho itakabidhiwa kombe lake hilo la 25 la ubingwa wa Bara na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, baada ya mechi hiyo na mabingwa hao wa Bara msimu wa 2013/2014
Comments
Post a Comment