KOCHA wa timu ya soka Taifa, ‘Taifa Stars’, Mart Nooij amesema watajitahidi kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano yote iliyoko mbele yao.
Taifa Stars ipo kwenye harakati za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) na ile ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Kwa sasa timu hiyo ipo kambini ikitarajiwa kucheza na Misri Juni 14 katika mechi ya kuwania kufuzu Afcon. Akizungumza jana kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa jezi na utoaji wa tuzo kwa waliotoa mchango kwenye soka ya Tanzania, Nooij alisema wana kikosi cha wachezaji 41 kambini ambapo baadhi wataondoka leo na wengine watabaki kujiandaa na michuano ya Chan.
“Tutajaribu kufanya vizuri, tuna Afcon na Chan yote ina umuhimu mkubwa kwetu, watakaobaki wataenda Zanzibar kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda,” alisema.
Kwa upande wake nahodha wa Stars, Nadir Haroub alisema uzinduzi wa jezi mpya utawasaidia wao kuzivaa na kwenda kupambana kwa juhudi ili kupata ushindi.
Kocha Nooij leo anatarajiwa kutaja kikosi kitakachoenda Ethiopia kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi dhidi ya Misri. Tangu kocha huyo ajiunge na Stars timu hiyo imekuwa haifanyi vizuri kwenye mechi zake mbalimbali, hali iliyopelekea wajumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF kumpa mechi tatu za kufanya vizuri, akivurunda atafutwa kazi.
Ofisa Habari wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao ndio wadhamini wa timu hiyo kupitia bia yao ya Kilimanjaro, Dorice Malulu alisema wanaitakia heri Taifa Stars katika maandalizi ya Afcon na kuahidi kutoa bonge la kiburudisho kwa timu hiyo.
Comments
Post a Comment