Published on Wednesday, 03 June 2015 00:07
Written by Mgaya Kingoba, Dodoma
Hits: 72
SERIKALI inaandaa programu maalumu ya kunasa kazi za wasanii zinazochezwa redioni, kwenye televisheni na katika simu kufahamu kiasi gani kinastahili kulipwa kwa kutumia kazi hizo ili kuongeza mapato ya wasanii na ya serikali.
Aidha, tangu kuanza kwa urasimishaji wa kazi za sanaa, hadi kufikia Mei mwaka huu, CD na DVD 30,984 zimekamatwa kwa kazi za ndani na 45,166 kwa kazi za nje.
Pia Serikali imesema maandalizi ya kurekebisha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya Mwaka 1999 imeanza na rasimu ya kwanza imeshaandaliwa.
Akizungumzia kifaa hicho, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janet Mbene alisema imetangazwa zabuni ya kutafuta programu hiyo ya kunasa kazi hizo kwa nia ya kujua kiasi gani anastahili kulipwa msanii na serikali.
Alisema stempu zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu urasimishaji wa sanaa uanze ni 45,570,000 kwa muziki na 18,420,000 kwa filamu, na taarifa kama hizo hazikuwepo kabla ya urasimishaji.
“Mfumo wa pamoja wa kielektroniki wa kushughulikia utoaji wa stempu ya kodi uliozinduliwa tarehe 25, Mei, 2015 utasaidia taarifa kupatikana kwa haraka juu ya utoaji wa stempu na vibali mbalimbali vitakavyotolewa na Cosota, Basata, Bodi ya Filamu na TRA kwa kazi husika,” alieleza Naibu Waziri.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM), Naibu Waziri alisema marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, yameanza kwa rasimu ya kwanza kuandaliwa baada ya kupata maoni na mapendekezo kutoka wadau wapatao 22.
Aliwataja wadau hao kuwa ni kutoka katika Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mawakili wa Serikali, waigizaji, wachapishaji, mawakala wa kujitegemea na mapromota.
“Aidha, Waraka wa Baraza la Mawaziri umeandaliwa ili kupata maamuzi ya serikali na pindi hatua itakapokamilika muswada husika utawasilishwa bungeni,” alisema Naibu Waziri
Comments
Post a Comment