SERIKALI imeombwa kuangalia upya Sheria ya mtoto ya mwaka 1971 kwani imebainika kuwa ndio chanzo kimojawapo kinachoruhusu na kuchangia ndoa za utotoni pamoja na mimba za utotoni.
Akizungumza katika wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Intiative for Youth (INFOY), Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wilaya ya Arusha, Hassani Omary alisema ni wajibu wa serikali kuangalia upya sheria hiyo kwani sheria hii imekuwa ikiwaathiri watoto wengi hapa nchini.
Alisema sheria hiyo imekuwa ikiruhusu watoto hata wenye umri chini ya miaka 18 kuolewa iwapo tu wazazi wake watakapokubali, kitu ambacho kinawaathiri watoto wengi katika masomo yao.
Alisema ikitokea mtu mmoja kupeleka lalamiko lake katika vyombo vya sheria amekuwa akishindwa kutokana na sheria hiyo kuleta mkanganyiko kwani mtoto huyo hata awe mdogo kuolewa mradi tu familia yake iwe imeafiki.
Aidha mbali na sheria hii pia Serikali inatakiwa kutilia mkazo katika mila mbalimbali na desturi kwani mila zingine zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa watoto wadogo hasa wa kike kukosa haki zao za msingi kwa kuwalazimisha kuolewa iwapo tu viongozi wa mila zao wakitaka huku akitolea mfano kwa kabila la kimasai ambalo wamekuwa wakisimamia na kulazimisha watoto wao kuolewa pindi atakapovunja ungo. Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa kulinda na kutetea haki ya sheria ya mtoto,
Laurent Sabuni alisema ni wajibu wa serikali kuangalia kwa makini sheria hiyo kwani imekuwa ikiwaathiri watoto na kuwakosesha haki zao.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Arusha, Saum Kweka alisema katika kipindi hicho ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anamlinda mtoto wake, anampa elimu mtoto wake kuhusiana na mimba za utotoni.
Comments
Post a Comment