WAKATI homa za wasanii mbalimbali juu ya shindano la Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) zikizidi kupanda, wadhamini wa shindano hilo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager, imeandaa kipindi cha runinga kitakachozungumzia juu ya tuzo hizo.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Meneja wa bia ya Kilimanajro Premium Lager, Pamela Kikuli, na kueleza kuwa kipindi hichi kitaitwa ‘Kili Chats.’
Alisema sio mara ya kwanza kwa bia hiyo kuandaa kipindi cha aina hii kwani mwaka jana kilirushwa wakati wa msimu wa ‘Nani Mtani Jembe’, kampeni inayowashirikisha wakongwe wa soka hapa nchini Simba na Yanga.
Meneja huyo alisema sasa hivi wameamua kujikita katika muziki kwani ndio msimu wa KTMA kwa hivyo wanataka kusikia kutoka kwa wananchi kuhusu maoni yao.
“Huu ni mwanzo mzuri kuelekea KTMA ambapo tutaalika wadau mbalimbali kwa mfano Ma DJ, wanamitindo, washiriki katika video mbalimbali na wengine,” alisema Pamela.
Alisema kipindi hicho kitarushwa na televisheni ya ITV kila Jumanne saa moja usiku hadi saa moja na nusu kuanzia Mei 12, mwaka huu.
Alisisitiza kuwa, wasanii hawatahusishwa katika kipindi hicho ili kuhakikisha wote wanapewa haki sawa kuelekea usiku wa tuzo.
“Wasanii hawatahusishwa kabisa kwa kuwa wao wanashindanishwa kwenye KTMA na wote tutajua matokeo usiku ule wa tuzo kwa hivyo hata kwenye kipindi hatutatoa maelezo yoyote kuhusu kura,” alisema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Pamela kipindi hicho kitatumika kutoa maelezo kuhusu namna ya kupiga kura.
Alisema hadhira (audience) itakayoshiriki katika kipindi hicho itapatikana kupitia ukurasa wa Kili wa facebook na kisha kupewa nafasi ya kushiriki wakati wa kuandaa show.
Fainali za Kili Music Awards 2015 zinatarajiwa kufanyika Dar es Salaam Juni 13 mwaka huu.
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager imedhamini tuzo hizi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 na ndio moja ya tuzo zilizodumu kwa muda na kujizolea umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kati
Comments
Post a Comment