MSAFARA wa watu 50 wa timu ya Yanga umeondoka nchini jana saa 5 usiku kwenda Tunisia kwa ajili ya mchezo wa hatua ya 16 bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel uliopangwa kupigwa Jumamosi usiku kwenye mji wa Sousse.
Katika msafara huo, Yanga imeondoka na kikosi cha wachezaji 20 kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kupitia Dubai kabla ya kwenda Tunisia, ambako ndipo yalipo makazi ya wapinzani wao Etoile.
Akizungumza na gazeti hili, kocha wa Yanga Hans van der Pluijm alisema wanakwenda Tunisia wakiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya hapa nchini ambayo anaamini yatawasaidia katika mchezo huo.
“Ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu, lakini hilo haliwezi kututisha na kukubali kirahisi tumejizatiti kuhakikisha tunapambana na kupata ushindi kama ambavyo wao walipata sare nyumbani,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema watahakikisha wanatumia mfumo wao waliozoea kucheza siku zote kwa kucheza kwa kasi na kutumia mawinga ili waweze kuwakimbiza mabeki wao ambao amegundua siyo wazuri hawana spidi kama ilivyo kwa wachezaji wake Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
“Tunataka kutengeneza mashambulizi mengi kwenye lango lao ili kupata bao moja ambalo litawapa mshtuko kwa sababu ya presha kutoka kwa mashabiki wao na baada ya hapo kazi yetu itakuwa nyepesi ya kuwadhibiti washambuliaji wao ambao ni hatari kwa mipira ya krosi,” alisema Pluijm.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Habari wa klabu ya hiyo, Jerry Muro aliwatoa hofu mashabiki wao na kuwataka kuwa na matumaini na kuendelea kuiombea timu yao ili waweke rekodi nyingine kwa kuwatoa mabingwa wa Afrika wa mwaka 2007 Etoile du Sahel.
Muro alisema kiwango cha timu yao kimewapa matumaini ya kuwatoa Etoile na wanakwenda Tunisia wakiwa na uhakika wa kuweka rekodi nyingine ya pili kwa mwaka huu baada ya ile waliyoiweka Jumatatu kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Tanzania Bara kwa mara 25 huku wakiwa wamebakiwa na mechi mbili mkononi.
“Mashabiki wa Yanga wanapaswa kutokuwa na hofu na badala yake kuiombea timu yao iweze kufanikisha malengo yao ya kucheza hatua ya makundi mwaka huu na kuendelea kufurahi kama walivyo furahia ubingwa wa Tanzania Bara Jumatatu wiki hii pale Uwanja wa Taifa,” alisema Muro.
Kikosi cha Yanga ambacho kimeondoka jana ni Deogratius Munishi, Ally Mustapha, Oscar Joshua, Juma Abduli, Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Rajab Zahiri, Said Juma, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Kpah Sherman, Edward Charles, Danny Mrwanda, Hussein Javu, Nizar Khalfan, Andrey Coutinho na Pato Ngonyani.
Yanga, inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili iweze kusonga mbele katika hatua ya makundi katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Aprili 18 Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment