KOCHA wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Mart Nooij amewaita wachezaji 16 kuingia kambini leo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017 huku mchezaji wa Mgambo JKT, Malimi Busungu akiitwa kwa mara ya kwanza.
Busungu ni miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri msimu uliopita katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni akiwa na mabao tisa.
Amekuwa akihusishwa kutaka kusajiliwa na klabu za Yanga, Simba na Azam Fc.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, Kikosi hicho kilichoitwa na Nooij kitaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma kupimwa afya zao na kujua maendeleo yao kabla ya kujumuishwa na kikosi kilichoshiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa).
Wachezaji wanaoingia kambini kupimwa afya ni Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga ), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo na Kelvin Friday (Azam FC).
Wengine ni Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand United), Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
“Mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika Kusini, Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokuwa kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji wengine waliopo kambini,” alisema.
Alisema wachezaji wote wataungana katika kambi ya pamoja Juni mosi 2015 kujiandaa na mechi hiyo itakayochezwa jijini Alexandria kwenye uwanja wa Borg El Arab, Juni 14, 2015.
Aidha, wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu pia watakuwepo kwenye kikosi kitakachokwenda Misri.
Kabla ya kuelekea nchini Misri, Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Juni 4, mwaka huu kwa muda wa wiki moja kabla ya kwenda Misri kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao
Comments
Post a Comment