estus Kilufi
MBUNGE wa Mbarali, Modestus Kilufi (CCM), amesema watendaji wala rushwa na mafisadi wanasababisha mawaziri waadilifu walaumiwe bila sababu.
Ametangaza vita na watendaji hao na wawekezaji katika jimbo lake ambao wanadaiwa kutaka kuyumbisha uamuzi wa suala la mipaka kati ya wananchi na hifadhi ya Ihefu katika Hifadhi ya Ruaha mkoani Mbeya.
Hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitangaza kuwa wananchi wataendelea kuishi katika maeneo yao baada ya kutatuliwa kwa mgogoro wa mpaka ulikuwapo kwa muda mrefu.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni jana kwa ukali, Kilufi alisema wapo watendaji mafisadi na wala rushwa wanaojali maslahi yao, ambao wanasababisha watu waadilifu walaumiwe bila sababu.
“Hapa Waziri (Nyalandu) analaumiwa bila sababu. Haya ni maamuzi ya Rais Kikwete, alikuja na Waziri Mkuu, na vikao vikafanyika na kufikia uamuzi huu. “Sasa kwa nini watu wakweli na waadilifu wanalaumiwa bila sababu? Kuna watendaji wala rushwa na mafisadi, wanachukua fedha kwa Waarabu na kusababisha matatizo haya,” alisema mbunge huyo.
Alisema watu hao wanawafahamu na kwamba wananchi wa Mbarali hawatakubali kitu kingine chochote, kwani huko nyuma watendaji hao walipewa Sh bilioni saba za kulipa fidia wananchi, lakini zikalipwa Sh bilioni mbili.
“Hawa ni watendaji wabovu wala rushwa. Hizi fedha nyingine zimekwenda wapi? Wananchi wangu wanataka fidia yao na waliochukua fedha hizi wamechukuliwa hatua gani,” alihoji Kilufi.
Alisema suala la Ihefu lilikwisha siku nyingi na kwamba wanachotaka sasa ni wananchi kulipwa fidia hiyo.
“Hatutakubali hapa, hifadhi imetukuta wananchi, watu wanachukua fedha kwa maslahi binafsi. Mbarali tutakuwa mfano. Hata kama sikupewa ulinzi, kama nikiuawa, wananchi wangu watajua mbunge wao amekufa kwa sababu gani, sitakubali,” alisema kwa ukali.
Aliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CCM), aliyesema kuna viongozi wanapokea rushwa na kusababisha matatizo katika jamii.
Alisema migogoro ya mipaka na maeneo ya uhifadhi inasababishwa na viongozi wasio waadilifu, na kuhoji watu wanaoingiza mifugo katika hifadhi huku wakiwa na silaha nzito, kuwa hao si wafugaji, bali majangili.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema ipo haja ya kuweka mazingira mazuri, tulivu na kodi zisizobadilika, ili kuongeza mapato ya utalii.
Aidha, Mbunge wa Kuteuliwa, Zakia Meghji (CCM), alipendekeza kuwapo kwa mkataba wa kubadilishana nembo ya tembo yaliyohifadhiwa na mataifa ya nje, akisema zinatumika gharama kubwa kulinda ‘tembo waliokufa’ sawa na zile zinazotumika kulinda walio hai.
Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii alisema yapo meno ya tembo tani 137 yaliyohifadhiwa ambayo yalikataliwa kuuzwa na taasisi ya kimataifa, na kuonesha hofu kuwa siku moja yanaweza kupotea na kusababisha mawaziri wafungwe.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), aliunga mkono hoja ya Meghji akisema meno hayo yanaweza kupigwa ‘dili’ kama yataendelea kuhifadhiwa
Comments
Post a Comment