SERIKALI na wafanyabiashara nchini wamefikia mwafaka juu ya matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs), kuendelea huku ikiendelea kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyojitokeza, ikiwa ni pamoja na ukokotoaji wa gharama za mfanyabiashara.
Mwafaka huo ulifikiwa baada ya Kamati ya Kitaifa, iliyoundwa kwa ajili ya kupitia na kubainisha changamoto mbalimbali kuhusu mashine hizo.
Mapendekezo ya kamati yalihusu kuongeza uwazi katika mfumo mzima wa kodi kwa mizigo itokayo nje ya nchi, kuanzia mchakato wa uthaminishaji na uondoshaji wa mizigo bandarini, utambuzi wa gharama za manunuzi ndani ya nchi na gharama za uendeshaji zisizotambulika kisheria kwa kutokuwa na stakabadhi.
Akizungumza jana Dar es Salaam mbele ya Kamati na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema baada ya kuanzishwa, utaratibu wa kutumika kwa mashine hizo, ulikutana na changamoto mbalimbali zilizosababisha kuibuka kwa malalamiko na migogoro katika jamii.
Alisema chini ya mwafaka huo, utasaidia kukusanywa kwa kodi kwa ufanisi, ikiwa ni katika kuingizwa kwa gharama za wafanyabiashara katika mashine hizo.
Mkuya alisema mashine hizo hazikuwa na tatizo, lakini mfumo mzima wa utumikaji wake ndio uliokuwa na changamoto kwa wafanyabiashara, ambapo suala la ukadiriaji nalo linafanyiwa kazi.
Alisema baada ya kufikiwa kwa muafaka huo, matumizi ya mashine hizo utaanza kukokotoa gharama za mfanyabiashara huku kukiwa na bidhaa 150, ambazo zitaainishwa gharama halisi za bidhaa hizo.
“Kule bandarini kumekuwepo na baadhi ya wakala wa kupakua mizigo bandarini ambao sio waaminifu ambao hujikuta wakitoa viwango tofauti vya gharama kwa wafanyabiashara pindi wanapokuwa wakikomboa mizigo yao,” alisema Mkuya na kuongeza kuwa mfanyabiashara hujikuta akipatiwa risiti tofauti na kiwango halisi kinachotakiwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja alisema kupitia mwafaka huo, uwazi na uwajibikaji katika matumizi za mashine hizo, utawekwa wazi, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi
Comments
Post a Comment