Jumanne Maghembe.
SERIKALI imesema kwamba sekta ya maji kwa kutumia mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imeongeza wananchi wanaopata huduma ya maji kutoka milioni 15.2 Juni, 2013 hadi kufikia milioni 20.9 sawa na asilimia 55.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge na Kambi Rasmi ya Upinzani wamepinga takwimu hizo. Aidha wabunge waliozungumza baada ya bajeti kusomwa jana, wabunge hao walisema kwamba kuna udanganyifu mkubwa wa takwimu zilizowasilishwa ndani ya Bunge, huku Kambi ya Upinzani ikidiriki kusema kwamba mipango ya Serikali ya kuwapatia wananchi wake maji imeshindwa.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Maji, Mohamed Rajab Mbarouk alisema kwamba takwimu za utafiti wa kitaifa katika eneo la maji, zinaonesha kwa sasa wananchi wanaopata maji safi na salama ni asilimia 40 tu na sio asilimia 57.8 kama ilivyorekodiwa katika taarifa za Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta).
Alisema takwimu nyingi pamoja na visima vinavyofanya kazi si sahihi, hali inayodhihirisha kwamba sera ya maji imeshindwa kufanikiwa.
Akizungumzia miradi ya maji vijiji kumi kwa kila wilaya inayofadhiliwa na Benki ya Dunia tangu mwaka 2007, Mbarouk alisema Serikali haina ilichofanya na kuwa asilimia 75 ya miradi hiyo imekwama.
Mafanikio ya Serikali Akiwasilisha bajeti yake ya Wizara ya Maji ambapo mipango ya maendeleo imeshuka kwa asilimia 12.6 ikilinganishwa na bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2014/15, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisema kufikia Aprili 2015 kulikuwa na ongezeko la wananchi milioni 5.76 wanaoishi vijijini ambao wameingia katika wale wanaopata huduma za maji safi.
Akiainisha mafanikio ya Wizara yake baada ya kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini kupitia mamlaka za maji kwenye Miji Mikuu ya Mikoa 23 pamoja na Dar es Salaam; Miji Mikuu ya Wilaya 99, Miji Midogo 14; na Miradi 8 ya kitaifa, Kwa sasa takribani watu milioni 7 wanapata huduma ya maji safi na salama kwa upande wa Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo pamoja na huduma inayotolewa na miradi ya kitaifa.
Vilevile, wakazi wapatao milioni 3 kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani wanapata huduma hiyo.
Akizungumzia suala la uzalishaji na mahitaji Waziri Maghembe alisema kwamba hadi mwezi Aprili mwaka huu, mahitaji ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa ni lita milioni 619 kwa siku ikilinganishwa na uzalishaji wa lita milioni 385 kwa siku.
Wastani wa wakazi wanaopata huduma ya maji katika miji hiyo kwa sasa ni asilimia 86 kwa wastani wa saa 17 kwa siku. Aidha idadi ya wateja waliounganishwa na huduma ya maji imeongezeka kutoka 336,898 mwezi Machi, 2014 hadi wateja 362,953 mwezi Aprili, 2015 huku asilimia 96 ya wateja waliounganishwa na huduma hiyo wamefungiwa dira za maji.
Aidha kufikia Aprili 2015, mahitaji ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo ni lita milioni 450 kwa siku ikilinganishwa na uwezo wa mitambo wa kuzalisha maji wa lita milioni 300 kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 77 ya mahitaji. Wastani wa asilimia 68 ya wakazi wa Jiji wanapata huduma ya maji kwa wastani wa saa 8 kwa siku.
Wakazi wanaobaki hupata huduma ya maji kupitia visima, magati na huduma ya magari (water bowsers). Aidha, idadi ya wateja waliounganishwa na huduma ya maji ni 126,405 na kati ya hao, asilimia 97 wamefungiwa dira za maji.
Alisema Waziri Maghembe kwamba makusanyo ya maduhuli kwa mwezi sasa ni Sh bilioni 3.31 na kiwango cha upotevu wa maji ni asilimia 57. “Upotevu huo unatokana na wizi wa maji, uvujaji wa mabomba , uharibifu unaotokea wakati wa ukarabati wa miundombinu ya barabara pamoja na uchakavu wa miundombinu,“ alisema.
Malalamiko Wabunge walipata nafasi ya kuzungumza walilia na utekelezaji wa bajeti ya 2014/15 ambayo walisema mengi yaliyoandikwa hayazingatii ukweli ulivyo katika maeneo husika.
Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa (CCM) alionya kwamba kama takwimu hazitumiki ipasavyo, zitatoa taarifa ambayo si sahihi kuhusu upatikanaji wa maji na kusema ni vyema ikaelezwa wazi idadi ya vijiji vyenye maji salama badala ya kutumia vigezo vya asilimia.
Mbunge huyo ambaye alishawahi kuwa waziri katika Serikali zilizopita alisema kwa kuvitaja vijiji itaeleweka wazi nani ana maji na nani hana maji na hivyo serikali ijayo ikajua wapi pa kuanzia au kuendelezea.
Aidha mbunge huyo alitaka kuwepo na vipaumbele katika miradi ya maji na kuikamilisha kwanza kabla ya kurukia mingine mipya na kuiacha zamani ikiwa haijamalizwa.
Alisema wizara haitapongezwa kwa kuja na miradi mipya lakini itapongezwa kwa miradi iliyokamilika alisisitiza. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Azza Hamad ( CCM) alisema miradi ya maji huko Isaka, Kagongwa na Tinde ilitengenezwa Sh bilioni 8 kwa mwaka wa sasa wa fedha, lakini mradi huo huo umetengewa tena fedha kiasi hicho hicho lakini katika upembuzi na kuuliza kulikoni.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) alisema Tanzania ndio nchi pekee iliyozungukwa na maji lakini watu wake hawana maji safi ya kutumia.
Alisema kelele za maji ni matokeo ya Wizara ya Maji kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa umma. Mbunge wa Nkasi, Ally Mohamed Kessy (CCM) yeye alisema wazi kwamba hauingi mkono hoja kutokana na kudanganywa mara nyingi na wizara hiyo.
Alisema hata taarifa zilizopo katika bajeti kwamba mradi wa King’ombe kwenye halmashauri aliyomo, ambapo waziri alisema unatoa maji katika viotuo 19 na watu 4,500 wana maji, hauna maji na wala ahuna vituo 19 vya kuchotea maji. Pia alisema mradi wa Matala unaodaiwa kuwa na vituo 23 vya kuchotea maji na kuwanufaisha watu 4,096 pia hauna ukweli.
Alimtaka waziri asiwe anasikiliza wataalamu wake ambao wengi wanamdanganya na kutembelea mwenyewe miradi hiyo aone ilivyo.
Upatikanaji wa maji Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo,Waziri Maghembe alisema hairidhishi, hivyo, Wizara yake kwa kushirikiana na TAMISEMI inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya maji na kuzijengea uwezo Mamlaka hizo ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi katika miji hiyo.
Aidha katika kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa maji wenye uhakika Wizara iliendelea na kusaka vyanzo mbalimbali vya maji kuviainisha, kufanyia tathmini na usanifu na kuanza kuvihifadhi.
Alisema Katika mwaka 2014/2015, jumla ya vyanzo vya maji 114 vilitambuliwa kwenye mabonde ya Ziwa Rukwa vyanzo 94, Ziwa Nyasa (17), Rufiji (1), Wami- Ruvu (1)na Ziwa Tanganyika. Aidha, maeneo 413 yalifanyiwa utafiti wa maji chini ya ardhi ili kubaini maeneo yanayofaa kwa ajili ya uchimbaji wa visima.
Katika mwaka 2015/16, Wizara imepanga kuchimba visima 20 na kukarabati visima 30 vya kuchunguza mwenendo wa maji chini ya ardhi, pamoja na kuendelea na taratibu za kutafuta fedha ili kuajiri wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa vyanzo vipya vya maji.
Waziri Maghembe katika hotuba yake iliyozungumzia pia miradi ya kitaifa ya kimkakati aliliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Sh 458,900,981,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara kwa mwaka 2015/16 watekeleze majukumu na malengo yaliyoelezwa katika hotuba.
Comments
Post a Comment