MSAFARA wa Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, umepata ajali wakati mwanasiasa huyo akiwa katika harakati za kutimiza masharti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kutafuta wadhamini ili aweze kuwania nafasi ya urais. Ajali hiyo iliyojeruhi watu watano waliokuwa kwenye msafara huo, ilitokea jana katika eneo la Tekniko, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma baada ya gari aina ya Land Cruiser lenye namba T 188 BXG walilokuwamo kupinduka. Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ferdinand Mtui, alisema ilitokea saa 10:30 asubuhi wakati msafara huo ukiongozwa na Makongoro ukielekea Kigoma mjini. Kamishna Mtui aliwataja waliojeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo kichwani na mabegani kuwa ni dereva wa gari hilo Julius Kambarage, ambaye ni mtoto wa Makongoro na mwandishi Evans Magege. Wengine ni Katibu Mwenezi wa CCM, Musoma Mjini, Fikiri Marumba na Ally Tesha a...